top of page
Search

Daikyo Heroes Yanasa Vifaa Tano kujiandalia ligi kuu ya Hoki

  • heartmediak4
  • Jul 19, 2024
  • 1 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 19 Julai 2024.



TIMU ya wanaume ya mchezo wa magongo ya Daikyo Heroes imenasa wachezaji watano kwenye juhudi za kujiandalia ngarambe ya ligi kuu msimu mpya. Daikyo Heroes yenye makazi yake katika jiji la Mombasa itakuwa inashiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza baada ya kupandishwa ngazi kwa kubeba taji la Supa ligi muhula uliyopita. Timu ya Chuo Kikuu cha Eldoret (UoE) pia ilipandishwa ngazi kushiriki ligi kuu baada ya kuibuka ya pili kwenye michuano hiyo.


Ofisa mkuu wa Daikyo Heroes, Farhan Khan ambaye ndiye nahodha, mfadhili pia mwanzilishi wa timu hiyo alisema wamechukua hatua hiyo ili kujiongezea nguvu. ''Ndio mwanzo wa ngoma kushiriki ligi kuu yenye ushindani mkali ambapo imebidi tusaka wachezaji wachache wazoefu ili kutuchochea kwenye kampeni hizo,'' alisema. Aliongeza kuwa ana imani huduma za watano hao zitazalisha matokeo mema kwenye mbio za kupigania taji hilo ambalo limetwaliwa na Butali Warriors kwa miaka minne mfufulizo. Imetwaa huduma zake Conrad Wafula (Western Jaguars), Derick Jabali (Kenya Police), mnyakaji Peter Apwacho (Mvita X1), Arif Shah (Butali Warriors) na Henry Otuoma akitokea Chuo Kikuu cha Kenya College Accountancy (KCA).


Khan anashikilia kuwa wamepania kushusha mchezo mzuri kama walivyotenda kwenye kampeni za Supa Ligi. Anadokeza kwamba anaamini wanatosha mboga kujituma kwa udi na uvumba na kufanikiwa kutawazwa mabingwa ndani ya msimu wa kwanza. Hata hivyo anakiri kuwa wanafahamu wanatarajia shughuli zito. Kamwe haitakuwa mteremko kwa kuzingatia ngarambe hiyo itajumuisha klabu ambazo zimekuwepo ligini kwa muda mrefu. Daikyo Heroes itakabili ushindani mkali mbele ya Butali Warriors, Kenya Police, Western Jaguars, Gladiators ya Chuo Kikuu cha Strathmore, Mashujaa ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha USIU-A na KCA kati ya zingine.

 
 
bottom of page