top of page
Search

Chipukizi Watesa Mchezo wa Bowling, Kjellan Ikitwaa taji la ASUS Cup

  • heartmediak4
  • Sep 3, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne, 3 Septemba 2024


TIMU za wachezaji wasiozidi miaka 40 zatamba mbele ya wenzao waliozidi miaka 50 kwenye shindano la mchezo wa Bowling (mpira wa bakuli) kuwania taji la (National Fours ASUS Cup). Ngarambe hiyo iliyoshirikisha timu za wachezaji wanne kila upande ilifanyika Jumapili Tarehe 1, Septemba 2024 ugani Ruiru Sports mjini humo.




Timu ya nahodha, Kjellan Awour ilitawazwa mabingwa baada ya kulemea timu ya nahodha, Andrew Johns kwa alama 18-15 katika fainali iliyoshuhudia ushindani mkali. Klabu nyingi za mchezo huu hushirikisha wachezaji wakongwe kuanzia miaka 50 lakini baadhi yazo zimezamia mpango wa kushirikisha wachezaji wa miaka ya chini. Timu nyingi za wakongwe zilibanduliwa katika robo fainali.



''Licha ya kupata ushindani mkali napongeza wenzangu kwa kujituma na kuhakikisha tumeibuka washindi,'' alisema Kjellan Awuor. Aliongeza kuwa ndio mara yake ya kwanza kuwa nahodha na kuibuka washindi. Alidokeza hayo maana amekuwa nahodha zaidi ya mara kumi kwenye mechi za wachezaji wawili, watatu na wanne lakini upande wake haujawahi kushinda.


Shindano hilo lilidhaminiwa na ASUS Computers kupitia mshirika wake nchini The Laptops Clinic. Ofisa mkuu wa The Laptops Clinic, Charles Mathenge Maina alishukuru wachezaji wote kwa kuonyesha nidhamu nzuri kwenye shindano hilo. ''Shindano hili limeonyesha wazi kuwa mchezo huu unaendelea kusamba na kuvutia wachezaji wa umri mdogo kinyume na miaka iliyopita,'' alisema. Aliongeza ataendelea kushirikiana na ASUS Computers kudhamini mashindano tofauti ya mchezo huo siku zijazo. Kadhalika alishukuru klabu ya Ruiru Sports Club kwa maandalizi mema.


Naye Rais wa Shirikisho la Mchezo huo (KB), Sophy Kihuyu alishukuru wadhamini wa kipute hicho kwa kuzingatia wachezaji wa timu za taifa wanaume na wanawake walikitumia kama maandalizi ya pambano la Afrika (AST) nchini Botswana baadaye mwezi huu.


Timu ya Kjellan Awour ilifuzu kwa fainali kwa kuzima timu ya Anwar Hamad kwa alama 20-18 nacho kikosi cha Andrew Johns kilizoa alama 18-09 dhidi ya Alex Mburu kwenye nusu fainali. Kinyang'anyiro hicho kilivutia timu 16 zilizojumuisha wachezaji 64 mchanganyiko wanaume na wanawake.

 
 
bottom of page