top of page
Search

Akhayo Anapania Kufuata Nyayo za Nduguye Stanley Okumbi

  • heartmediak4
  • Jul 27, 2024
  • 3 min read

Na HEART MEDIA

Jumamosi, 27 Julai 2024.


KOCHA Jeremiah Akhayo hunoa makucha ya wachezaji wa klabu za viwango vya chini, lakini anapania kufunza timu za haiba kubwa nchini hasa kwenye Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka ya Kenya (FKF-PL) miaka ijayo. Kocha huyu sasa ni naibu wake kocha, Geoffrey Wangalwa wanakonoa timu ya Kariobangi Legends Youth inayoshiriki mechi za FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL).


Akhayo ambaye ni mdogo wake kocha wa zamani wa Harambee Stars, Stanley Okumbi alivutiwa pia alikuwa akishiriki fani kadhaa akisoma Shule ya Msingi na Upili. ''Kipindi hicho nilikuwa nashiriki Soka, Tae Kwo Ndo, Karate na Masumbwi,'' anasema. Anaongeza kuwa hali hiyo ilichangia kuteuliwa kiranja wa michezo akisoma Shule ya Msingi na Sekondari. Akiwa Dandora Secondary ingawa hakuwa akifanya vizuri katika soka mara mbili alichezea timu ya Shule hadi kiwango cha kitaifa.

Baada ya kukamilisha elimu ya sekondari kimasomo hakuweza kuendelea ambapo alianza kushiriki Tae Kwon Do alikochezea timu ya Huduma ya Vijana Kwa Taifa (NYS) na Mathare Depot.


''Katika Tae kwon Do nakumbuka nikiwa sekondari niliteuliwa mara mbili kuchezea timu ya taifa ambapo nilishiriki shindano la Kombe la Dunia nchini Malaysia na Japan,'' anasema. Kisha baada ya kutamatisha elimu yake akichezea NYS kwa mara ya tatu aliteuliwa katika timu ya taifa alikoshiriki shindano la Kombe la Afrika nchini Uganda. Aliamua kutema Tae Kwon Do mwaka 2012 na kugeukia soka.




Hata hivyo anasema kuwa alianza kufunza soka angali mwanafunzi wa Shule ya Msingi kwani alikuwa akiongoza wenzake kwa kuwapa mawaidha kuhusu mchezo huo. Anashikilia kuwa uongozi wake ulianza kutambuliwa kipindi hicho. Vile vile enzi hizo alikuwa anafunza timu ya Samba Youth kwa wasiozidi umri wa miaka U10, U12 na U14 mtaani Dandora. Timu hizo zilikuwa zikishiriki ligi za MYSA ambapo timu ya U14 ikibeba taji hilo ilikuwa inafuzu moja kwa moja kushiriki shindano la Afrika Mashariki ambapo alishiriki mara mbili.



Aidha anajivunia kuongoza Acakoro Academy iliyoanzishwa na Stanley Okumbi ambapo mara mbili ilishiriki shindano la Donauauen Cup, Linz Austria. ''Mwaka 2015 niliongoza Acakoro Youth kitengo cha wavulana kubeba taji hilo baada ya kuzamisha Barcelona kwa bao 1-0 katika fainali,'' akasema. Kwenye mechi hizo walikuwa wamecheza dhidi ya Juventus, Liverpool na Atletico. Mara ya pili walishiriki mwaka 2018 lakini hawakufanya vizuri kwani walimaliza nafasi ya saba. Kadhalika anajivunia kuchezea na kunoa Korogocho Youth bado ilianzishwa na Stanley Okumbi tangia mwaka 2012 hadi 2014. Kipindi hicho ilikuwa inashiriki Ligi ya Kaunti, Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL) na Ligi ya Taifa Daraja la Pili. Kwa sasa Korogocho Youth ilibadilishwa jina ambapo inafahamika kama Rainbow FC.



Ingawa alijunga na Kariobangi Legends Youth mwezi Mei 2024, bado ananoa timu ya wachezaji chipukizi ya Acakoro kwa wasiozidi umri wa miaka 14 wavulana na wasichana. Pia kwa mwaka wa pili ndiye kocha wa Kariobangi Sports inayoshiriki ligi ya Kaunti ya Nairobi chini ya FKF Kanda ya Nairobi Mashariki. Amepania kusomea ukufunzi levo B kwani amehitimu kwa levo D na C.

Katika mpango mzima anashikilia kwamba kwa jinsi wachezaji wa Kariobangi Legends Youth wanavyopiga soka la kibiashara wamekaa pazuri kutwaa ubingwa wa Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki na kupanda ngazi. Katika msimamo wa kipute hicho, Kariobangi Legends Youth inaongoza kwa alama 79, tisa mbele ya Lucky Summers kwa kushuka dimbani mara 31 na 32 mtawalia. Utawala Youth inashikilia tatu bora kwa alama 66, mbili mbele ya Babadogo United.


Anashauri wachezaji wanaokuja kuwa nyakati zote lazima wajitume kiume pia kujiwekea malengo ya kupiga hatua na kuonyesha nidhamu nzuri. ''Nidhamu ndio msingi wa mchezaji yeyote kutambuliwa na kushikwa mkono katika taaluma yake,'' akasema.

Shule ya Msingi alisomea Ngomongo na kumalizia Good Neighbours mtaani Dandora. Kisha sekondari alisomea Dandora mwaka 2006 hadi 2009.

 
 
bottom of page