top of page
Search

44 Legends Yaona Giza Ugenini Japo Kirafiki

  • heartmediak4
  • Oct 15, 2024
  • 1 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne, 15 Oktoba 2024



TIMU ya 44 Legends ilirejea makwao mikono mitupu ilipobamizwa kwa mabao 2-0 na wenyeji wao Kariobangi Legends Wazee kwenye patashika ya kupimana nguvu iliyopigiwa uwanja wa Kariobangi North Primary, Embakasi Nairobi. Mechi hiyo iliyochezwa Jumapili tarehe 13, Oktoba ni kati ya misururu ya michuano ya Kariobangi Legends Wazee inayoendelea kutetemesha wapinzani wao.


Kariobangi Legends Wazee inajivunia kumaliza ya pili kwenye ligi ya wazee pamoja Kaunti ya Nairobi msimu uliyopita. Nayo ABSA Legends ilijitahidi kiume na kuhifadhi ubingwa huo iliyokuwa imetwaa muhula uliyotangulia.

Kwenye patashika ya juzi, wachezaji wa Kariobangi Legends chini ya kocha, Philip Munyoki walipata mtihani mgumu mbele ya wageni wao lakini mwishowe walifanya kile wamezoea.



Wachana hyavu hao walikaza buti bila kuhofia wapinzani wao na kupata bao la kwanza kupitia Hillary Otieno ambaye ndiye meneja wa Kariobangi Legends Youth. Goli la pili lilitupiwa kimiani na Geoffrey Wangalwa aliyekuwa kocha mkuu wa Kariobangi Legends Youth.

''Kama kawa huwa hatuna la ziada bali tunastahili kushinda mechi zote tunazoshiriki maana wachezaji wote wanafahamu mbinu za kusakata kabumbu,' anasema meneja wa Kariobangi Legends, Julius Agwaya. Anashikilia kwamba kikosi chake kinajumuisha wachezaji ambao ni makocha wa timu zingine pia waliowahi kuchezea vikosi vingine ikiwamo kupigia timu ya taifa.



Naye meneja wa 44 Legends, Charles Mwai anasema kuwa licha ya kupoteza mchuano huo wanazidi kujifunza mengi. ''Bila shaka kwa kila mechi huwa tupo makini zaidi hasa tujifunze kitu ili kurekebisha makosa yetu kwenye mechi zijazo,'' anasema. Anaongeza kuwa kupoteza mechi sio tatizo bali ni funzo kwa wenye wanaolenga kuboresha mchezo wao. Kariobangi Legends Wazee inazidi kunyamazisha wapinzani wanaokutana nao dimbani. Wiki iliyopita ilitwaa ufanisi wa magoli 6-1 dhidi ya Mathare North Legends.

 
 
bottom of page